Genesis 26

Isaka Na Abimeleki

1Basi njaa kubwa ikawa katika nchi hiyo, kuliko ile njaa iliyotangulia iliyotokea wakati wa Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki mfalme wa Wafilisti huko Gerari. 2Bwana akamtokea Isaka, akamwambia, “Usiende Misri, bali ukae katika nchi nitakayokuambia. 3Kaa katika nchi hii kwa kitambo, mimi nitakuwa pamoja na wewe na nitakubariki. Kwa maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote na nitatimiza kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. 4Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote na kutokana na uzao wako mataifa yote yatabarikiwa, 5kwa sababu Ibrahimu alinitii mimi akatunza kanuni zangu na maagizo yangu, amri zangu pamoja na sheria zangu.” 6Hivyo Isaka akaishi huko Gerari.

7Watu wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Watu wa mahali pale wataweza kumuua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa alikuwa mzuri wa sura.”

8Wakati Isaka alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona jinsi Isaka alivyomkumbatia Rebeka mke wake. 9Abimeleki akamwita Isaka akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu?’ ”

Isaka akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.”

10Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotufanyia? Ingewezekana mtu yeyote akawa amekutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia juu yetu.”

11Hivyo Abimeleki akatoa amri kwa watu wote, akisema, “Yeyote atakayemnyanyasa mtu huyu au mkewe hakika atauawa.”

12Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. 13Isaka akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. 14Akawa na mifugo ya kondoo na ng’ombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. 15Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Ibrahimu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo.

16Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.”

17Basi Isaka akatoka huko akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko. 18Ndipo Isaka akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Ibrahimu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya kufa Ibrahimu, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa.

19Watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde wakagundua huko kisima chenye maji safi. 20Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki,
Eseki maana yake ni Ugomvi.
kwa sababu waligombana naye.
21Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania, akakiita Sitna.
Sitna maana yake Upinzani.
22Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi,
Rehobothi maana yake ni Mungu ametufanyia nafasi.
akisema, “Sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.”

23Kutoka pale akaenda Beer-Sheba. 24Usiku ule Bwana akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Ibrahimu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe, nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.”

25Isaka akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima.

26Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake. 27Isaka akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu na ninyi mlinichukia na kunifukuza?”

28Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwa Bwana alikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu, kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe 29kwamba hutatudhuru, kama jinsi nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote na kuwaondoa kwetu kwa amani. Tena sasa umebarikiwa na Bwana.’ ”

30Basi Isaka akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa. 31Kesho yake asubuhi na mapema, wakaapizana wao kwa wao. Kisha Isaka akawaruhusu waende zao, wakamwacha Isaka kwa amani.

32Siku hiyo watumishi wa Isaka wakaja wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!” 33Naye akakiita Shiba,
Shiba kwa Kiebrania maana yake ni Saba.
mpaka leo mji huo unaitwa Beer-Sheba.
Beer-Sheba maana yake ni Kisima cha wale saba, yaani wale kondoo saba ambao Ibrahimu aliwatoa kama ushahidi kati yake na Abimeleki.

34Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti. 35Hawa walikuwa chanzo cha huzuni ya Isaka na Rebeka.
Copyright information for SwhKC